Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Sayyid Muqtada Sadr, kiongozi wa Harakati ya Kitaifa ya Kishia nchini Iraq, siku ya Jumatano alionesha hasira na kutoridhishwa kwake kutokana na kauli za Irfan Siddiq, Balozi wa Uingereza mjini Baghdad, Siddiq alikuwa amedai kwamba; nchi yake baada ya kuanguka kwa utawala wa zamani katika msimu wa masika ya mwaka 2003, iliukabidhi uongozi wa serikali kwa Mashia nchini Iraq.
Muqtada Sadr aliandika katika mtandao wa “X” akimlenga Balozi wa Uingereza kwa kusema: Ikiwa kuna kundi la Mashia waliojitokeza mbele yenu, basi sisi si miongoni mwao, na kamwe hatutakuwa miongoni mwao duniani wala Akhera.
Aidha, akimuuliza balozi huyo alisema: Je, mmesahau ni nani aliyemleta dikteta huyo mharibifu?
Akimlenga balozi huyo aliendelea kusema: Huenda pia mmesahau kwamba mlitoroka mbele ya harakati pekee ya Muqawama iliyosimama dhidi yenu ili kuiweka huru nchi yake kutoka mikononi mwenu, hususan katika jimbo la Basra.
Pia alirejelea nafasi ya “Harakati ya Sadr” katika kupinga utawala huo kutoka ndani ya nchi pamoja na kuiweka huru nchi dhidi ya utawala wa kigeni.
Muqtada Sadr aliituhumu London kwamba; siku zote imekuwa na bado ni mahali salama kwa wanachama wa Chama cha Baath, watu waliopenyezwa pamoja na hata maadui wa dini, madhehebu na taifa.
Alisema kuwa; vituo vyao vya habari ni ushahidi wa jambo hilo, na akaitaka serikali ya Uingereza kuwapeleka watu hao wote kwa haraka mbele ya mfumo wa haki wa Iraq, pia alitaja uwepo wao kuwa ni “pengo la kisiasa na kidiplomasia.”
Kiongozi wa Harakati ya Sadr pia aliitaka London kuomba radhi rasmi kutokana na kauli za hivi karibuni za balozi wake kwa mujibu wa taratibu za kawaida za kidiplomasia, huku wakati huohuo akisisitiza kukataa aina yoyote ya utawala wa kigeni bila kujali asili yake.
Maoni yako